Kuku wa nyama

Hawa ni kuku wanaofugwa kwaajili ya nyama. Kuku wa Kenchic kama chaguo, ni walaji wazuri na wanakua haraka sana. Wanakua tayari kwa kuuzwa katika umri wa wiki 4 mpaka 5, wanapokua na uzito wa kilo 1.5 mpaka 3. Kuku wako wataweza kupata upeo wa uzito huu kama utawalisha kwa usahihi.

Kuku wa nyama ni biashara yenye faida na manufaa, hata hivyo, sababu inayofanya wafugaji wengi wa kuku wa nyama kutofanikiwa au kupata hasara, ni kwasababu wanaanza bila mpangilio wa biashara. Hiki ni kitu cha kwanza na moja wapo ya vitu muhimu wanavyohitaji kupanga.

Mpango mzuri wa biashara utaonyesha malengo unayotarajia kufanikisha na jinsi unavyopanga kufikia huko. Pamoja na hayo itakuruhusu kujua soko lako kabla ya kuanza ufugaji halisi wa kuku wa nyama. Unaweza kufanya mipango ya uuzaji kwenye hoteli mitaani, mashule, migahawa,mkahawa,madukani na watumiaji wengine wa mara kwa mara.

Kama utajua soko lako kabla ya kuanza biashara yako utakua na uhakika wa kuuza kuku wako wa nyama mara tu wanapokomaa na kuwa na biashara yenye mafanikio.

Lazima pia uweke kumbukumbu nzuri za ufugaji na mahesabu ya uendeshaji wa biashara yako. Hii itakufanya ufatilie kama unatengeneza faida au la.